Siku chache zilizopita kumeibuka maswali mengi juu ya nini hufanya biashara kufa na nini hufanya zifanikiwe. Maswali haya yamekuja baada ya Mr Dominic Mmasi (@dominic_mmasi), mwanzilishi na mwendeshaji wa biashara ya Room of Jeans kufanya mahojiano katika jukwaa la "LetsImpactMillions" huku akisisitiza wafanyabiashara kuwa na mfumo/system itakayowaletea wepesi wa kuendesha biashara zao hata pasi na usimamizi wa karibu kila dakika. Ni wazi kuwa Dominic amejipata katika soko la Tanzania kwani amejenga brand kubwa sana katika uuzaji wa nguo aina ya Jeans, hivyo sio rahisi kupuuza kile anachosema kuwa ni chanzo cha mafanikio yake katika biashara. Dominic anadai kuwa moja ya vitu vilivyochangia mafanikio yake ni kuwa na mfumo mzuri wa biashara huku akikiri kujifunza kutoka kwa mfanyabiashara mwingine nguli na aliyefanikiwa sana, Mr Fredi Vunja Bei (@vunja_bei), aliyefanya naye kazi miaka kadhaa iliyopita.
Kabla sijaenda mbali, naomba nitolee maelezo maswali ambayo huenda yapo mbele yenu: Wavuka ni nini, na wanavuka kwenda wapi? Kama ulikuwa na maswali kama hayo, nikutoe wasiwasi kwani ni maswali ya msingi sana.
Kabla ya yote tuwatoe wasiwasi, bado tunajitafuta na hatujajipa kibali cha kutoa ushauri wa kibiashara. Aitha tunashiriki haya ili kushirikisha moja au mbili kutokana na uzoefu wetu mdogo tuliojifunza njiani, tukitumai kuwa nawe maomaji wetu jambo moja au mawili ambayo tunahakika nayo kutokana na uzoefu wetu wa miezi miwili tukijenga soko la magari Tanzania :)
Wavuka ni soko la magari nchini Tanzania ambalo bado linakua na linalenga kurahisisha ununuaji na uuzaji wa magari nchini. Kwa miaka mingi, soko la magari nchini Tanzania limekuwa likiendeshwa na watu wachache wenye taarifa za magari yaliyopo sokoni na thamani yake, maarufu kama Madalali. Wateja wenye uhitaji huwatumia wao ili kupata taarifa na mwisho wa siku kununua ikiwa wataridhishwa na hali ya gari pamoja na gharama zake baada ya ukaguzi. Watu hawa wamefanya kazi nzuri sana kwani soko limeendelea kukua na kujipatia umaarufu mkubwa. Kongole nyingi ziwaendee.
Lengo la Wavuka ni kuendeleza juhudi hizo kwa kurahisisha zaidi upatikanaji wa taarifa za magari sokoni. Tunalenga kurahisisha uelewa wa magari yaliyopo sokoni, thamani yake, na kuwapa wateja uwezo wa kuangalia machaguo (options) mbalimbali kabla hawajaamua kununua. Tunashukuru kuwa tangu tuanze, tumepokea mapokezi mazuri kutoka kwa wauzaji wakubwa nchini ikiwemo Africars, Tambuu Motors, Bingwa wa Magari Used, na wengine wengi. Yote hii inatutia moyo kwamba thamani yetu ni dhahiri.
Licha ya hayo yote, bado upo mlima mrefu wa sisi kuwafikia wanunuzi. Lengo letu si kuwa tu sehemu ambapo watu wanaponunua magari, la hasha! Tunatamani sana kuwa soko kamili kama masoko mengine. Sokoni huwa na watu wanaotembea tu kuangalia bidhaa (window shopping), na wengine huenda sokoni kujifunza na kupata upeo mpya. Hivyo basi, tunalenga kuwapa watu uwazi wa taarifa za magari, elimu, na urahisi wa kuelewa soko ili hata siku wakiamua kununua, wajue wapi waanzie.
Nimeongea mengi, lakini lengo langu kuu leo ni kuongelea timu iliyo nyuma ya Wavuka. Tumekuwa tukipiga hatua nyingi na za haraka kuzidi matarajio yetu, na hii yote isingewezekana kama si umahiri na umaridadi wa timu iliyo nyuma ya mradi huu.
Kipekee kabisa, niseme asante sana timu nzima nyuma ya Wavuka kwa kujitoa kwenu, juhudi, na ueledi mnaouonyesha kila siku. Hadi hii leo Tuna wastani wa watembeleaji 50 kwa siku, watu wenye account hai 110+, Wauzaji halali zaidi ya 20, Magari yaliyopo sokoni takribani 450+, Wafuassi wapatao 1000 kwatika mitandao yetu ya kijamii, watazamaji wapatao 50,000 kila mwezi katika mienzi miwili tangi tuanze. Kazi yetu bado ni kubwa lakini kama vile mwandishi wa tenzi anasema (we are gaining ground)— kazi yenu ni ya mfano na asanteni sana kwa kuendelea kupambana kujenga soko la magari lenye kuaminika na kuhudumia jamii kikamilifu.
Hivyo basi, katika kujibu lile swali nililoanza nalo juu ya mfumo mzuri wa biashara, sina mashaka kwamba moja ya mambo makuu yanayounda mfumo huo ni watu sahihi. "Watu sahihi" huenda ikawa ni neno pana, lakini kwa uzoefu wangu, watu wanakuwa sahihi katika biashara endapo wanakidhi sifa zifuatazo:
- Maono ya Pamoja (Shared Vision): Timu sahihi haifanyi kazi kwa ajili ya kukamilisha ratiba tu, bali kila mmoja anaelewa vyema mwelekeo wa kampuni/biashara na yupo tayari kupambana kufikia lengo kuu moja.
- Umahiri na Utayari wa Kujifunza: Watu wana ujuzi wa kutosha kwenye maeneo yao au wana unyenyekevu na kiu ya kujifunza mambo mapya kila siku kulingana na kasi ya soko.
- Uwazi na Uaminifu: Watu sahihi wanajenga mazingira yanayoruhusu kukosoana kwa staha, kupeana mrejesho, na kuaminiana bila haja ya kusimamiwa kila sekunde.
- Uthabiti na Kuhimili Changamoto (Resilience): Safari ya ujenzi wa biashara ina milima na mabonde; timu sahihi haikati tamaa mapema pindi mambo yanapokwenda tofauti na mipango.
Nina imani kuu kwamba Mr Dominic pamoja na Fred Vunjabei wataungana nami katika msimamo huu kuwa bila sifa hizi, mfumo wowote wa biashara, hata uwe mzuri vipi ni ngumu kuipelekea biashara kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Je, kwa upande wako unafikiri ni sifa gani nyingine kuu inayofanya timu kuwa "sahihi" kwenye biashara inayochipukia? Au ni uzoefu gani umeupata kwenye ujenzi wa timu katika biashara yako? Dondosha maoni yako hapo chini, au watumie team members wa biashara yako uwape mauwa yao